Vitunguu vinashambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali na kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo kwanza shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi.
MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU WA VITUNGUU
Vitunguu vinashambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali na kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo kwanza shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua hatua za kuzuia kabla uharibifu mkubwa haujatokea.
MAGONJWA YA VITUNGUU
a) Baka zambarau (Puple Blotch)
Ungonjwa huu unasababishwa na kuvu (fangasi). Chanzo kikubwa cha ugonjwa ni mbegu zenye ugonjwa. Pia ugonjwa unajitokeza wakati kuna ukungu na unyevunyegu mwingi hewani has wakati wa masika. Kiasi cha 60-80 % ya mazao yanaweza kupotea kama ugonjwa hautadhibitiwa.
Dalili za ugonjwa ni:-
· Kujitokeza madoa meupe yaliyodidimia kwenye majani na kwenye mashina ya mbegu
· Rangi ya zambarau kuwepo katikati ya doa jeupe.
· Majani kuanguka
· Mashina ya mbegu kuanguka kabla ya mbegu kutengenezwa
Baka Zambarau kwenye majani ya vitunguu |
Njia za kudhibiti:-
· Kupanda mbegu safi
· Kupanda vitunguu kwa kutumia mzunguko wa mazao
· Kuteketeza msalii ya vitunguu baada ya kuvuna
· Kupulizia dawa zilizopendekezwa kama Dithane M45 na Ridomil MZ. Dawa hizi zinachanganywa na povu la sabuni ili zijishike kwenye majani.
b) Ubwiri vinyoya (Downy Mildew)
Ugonjwa huu unasababishwa na kuvu (fangasi) na kuenezwa na mbegu, hewa na masalia ya vitunguu.
Unajitokeza wakati kuna unyevunyevu mwingi hewani hasa wakati wa masika na dalili zake ni kama zifuatazo:-
· Madoa yenye umbo la yai, rangi ya njano iliyofifia hujitokeza kwenye majani makukuu na kusambaa mpaka kwenye majani machanga.
· Baada ya siku chache madoa ya njano yanafunikwa na ukungu wa rangi ya kijivu.
· Majani yanasinyaa na kufa kuanzia kwenye ncha.
· Shina la mbegu huzungukwa na vidonda na kusababisha kichwa cha mbegu kuanguka.
Ugonjwa wa ubwiri vinyoya kwenye vitunguu |
Njia za kudhibiti ugonjwa ni kama zifuatavyo:-
· Kupanda mbegu safi
· Kupanda vitunguu kufuata mzunguko wa mazao
· Kupulizia dawa za ukungu kama dithane m45 na ridomil mz.
· Kuweka shamba safi
· Kuteketeza mabaki ya vitunguu
· Kumwagiliaji maji nyakati za asubuhi au jioni
c) Kinyausi (Damping – off)
Ugonjwa huu unasababishwa na fangasi na kuenezwa na udongo, mbegu na masalia ya mazao. Ugonjwa huu unasababisha mbegu kuoza kabla ya kuota na kunjauka kwa miche baada ya kuota. Ugonjwa unajitokeza hasa kitaluni ikiwa hali ya hewa ina unyevunyevu na udongo una maji maji.
Njia za kudhibiti ni kama zifuatazo:-
· Mbegu ziwe safi na ziwekwe dawa ya thiram
· Kutumia mzunguko wa mazao
· Kusia mbegu kwa nafasi za kutosha
· Kuepukana na kubananisha miche kitaluni
· Kuepukanana na kumwagilia maji wakati wa jua kali au wakati kuna ukungu
d) Virusi njano vya vitunguu (Onion yellow Dwarf virus)
Ugonjwa huu unasababishwa na virusi na kuenezwa na wadudu aina ya vidukari (wadudu mafuta).
Dalili za ugonjwa ni:-
· Mistari ya rangi ya manjano kwenye majani.
· Kujikunja kwa majani
· Majani kugeuka rangi ya manjano na kuanguka
· Mimea mzima kudumaa, kujikunja na kufa.
Virusi njano kwenye vitunguu |
Njia za kudhibiti ugonjwa huu ni:-
· Kutumia mbegu safi
· Kuweka shamba katika hali ya usafi
· Kuzuia wadudu kwa kupulizia dawa kama selecron, actellic, dursban nk.
WADUDU WAHARIBIFU WA VITUNGUU
Wadudu wanaosababisha uharibifu mkubwa kwenye vitunguu ni chawa wekundu (thrips) na sota (cutworms). Wadudu wengine ni pamoja na utitiri wekundu (red spider mites) na vipekecha majani (leaf miner)
a) Wadudu chawa (thrips)
Uharibifu uletwao na wadudu chawa, unatofautiana msimu mmoja na mwingine kutegemeana na hali ya hewa. Mvua kidogo pamoja na joto kali unasababisha mlipuko wa wadudu. Wanshambulia majani kwa kukwaruakwarua na kunyonya maji hivyo kusababisha majani kuwa na rangi ya fedha/siliver na baadaye majani yanakauka. Upungufu mkubwa wa mazao unatokea.
Wadudu chawa (thrips) kwenye majani ya vitunguu |
Njia ya kudhibiti hawa wadudu ni:-
· Kuweka shamba katika hali ya usafi
· Kuondoa magugu shambani na yanayozunguka shamba la vitunguu
· Kupulizia dawa ya wadudu kama karate, selecron, dursban, actellic.
b) Sota (Cutworms)
Sota au viwavi wa nondo wanasababisha uharibifu mkubwa. Viwavi wanakata mashina ya miche michanga sehemu ya chini ya shina juu ya ardhi. Sota wanapendelea kula wakati wa usiku na mchana kujificha kwenye ardhi karibu sana na sehemu waliokata shina. Uharibifu huu unapunguza sana idadi ya mimea shambani na kuleta upungufu wa mazao. Wadudu hawa wanadhibitiwa kwa kupulizia dawa kama; Karate Dursban na Actellic na kuweka shamba katika hali ya usafi.
Sota kwenye jani la kitunguu |
c) Utitiri wekundu (Red spider mites)
Hawa ni wadudu wadogo sana, ambao wanajificha upande wa chini wa majani. Wanafyonza maji maji kwenye majani na kusababisha majani kuwa na rangi nyeupe. Wadudu hawa wanatengeneza utando mweupe kuzunguka majani na mashina. Mmea unashindwa kutengeneza chakula na baadaye inakufa.
Utitiri mwekundu |
Njia ya kudhibiti:
· Kupulizia dawa za wadudu Karate na Selecron.
· Kuteketeza masalia ya mazao
· Kutumia mzunguko wa mazao
d) Vipekecha majani (leaf miner)
Hawa ni aina ya inzi wadogo, ambao viwavi wake wanashambulia majani, kwa kupekecha na kutengeneza mitandao wa mitaro kwenye majani. Viwavi wanashambulia majani na kusababisha majani kukauka. Upungufu mkubwa wa mazao hutokea.
Athari ya vipekecha majani |
Njia ya dhibiti:
· Kupulizia dawa ya wadudu kama karate Selecron na Dursban
· Kuteketeza masalia ya mazao
· Kutumia mzunguko wa mazao
No comments:
Post a Comment