KILIMO HIFADHI CHA MATANDAZO NA KUPANDA BILA KULIMA. - KILIMO NA UFUGAJI

Latest

Karibu uweze kujifunza na kujipatia elimu kuhusiana na kilimo na ufugaji ambapo utajifunza mbinu bora za kilimo na ufugaji pia utajifunza dondoo mbalimbali na mbinu bora na za kisasa za ufugaji

Sunday, October 8, 2017

KILIMO HIFADHI CHA MATANDAZO NA KUPANDA BILA KULIMA.

Katika mfumo wa uchumi wa soko huria, mkulima wa Tanzania hana budi kushindana kwa kuzalisha mazao kwa wingi na kwa gharama ndogo. Inampasa kila mzalishaji kutafuta na kutumia mbinu na maarifa zaidi katika uzalishaji.
Uchumi wa soko huria umesababisha ongezeko kubwa la gharama za mbolea za viwandani, zana, madawa ya kuulia wadudu pamoja mbegu bora. Katika hali hii ni wazi wakulima ( hasa wadogo wadogo ) hawataweza kumudu ushindani iwapo wataendelea kutumia pembejeo za viwandani.
Uharibifu wa mazingira ( mmomonyoko wa ardhi, mgandamano wa udongo au udomgongo mfu ) unachangiwa na ongezeko la watu pamoja na gharama kubwa ya zana na pembejeo. Tunalazimika kubadilisha mtazamo wetu juu ya mazingira na mfumo sahihi/endelevu wa Kilimo. Zipo njia za asili za kurutubisha udongo na vilevile Kilimo cha jadi cha kutunza mazingira.
Wakulima wanashauriwa kupunguza utegemezi wa mbolea za viwandani kwa kujitengenezea mbolea yao wenyewe mashambani kwa kupanda na kufunika ardhi kwa mimea ya mikunde.
MATANDAZO.
Matandazo ni mimea hai au mabaki inayopandwa kwa madhumuni ya kufunika udongo mwaka mzima.
Kanuni ya kufunika udongo kwa mimea jamii ya mikunde, nyasi na mingineyo ndiyo muhimu zaidi na ya msingi kuliko zote.
Mizizi ya matandazo ina uwezo wa kutindua na kulainisha udongo kwa kiwango kikubwa zaidi ya majembe tunayokatulia. Kilimo cha matandazo kinaondoa ulazima wa kukatua.
KUPANDA BILA KULIMA.
Inawezekana kupanda kwenye matandazo bila kuyalima kwa kutumia zana maalum. Hizi ni pamoja na Mwuo ( Dibbler ), Jembe la mkono, Kipanzi mkono ( Jab Planter), Kipanzi komoleo matandazo ( Direct seeder ).
KANUNI ZA KILIMO HIFADHI MATANDAZO.
- Funika udongo wakati wote kwa mimea hai au mabaki yake.
- Usichome moto, usihamishe mabaki ya mazao, usichungie mifugo holela.
- Usilime/uaikatue udongo.
- Panda kwa kukomelea kwa zana maalum.
- Kilimo cha mzunguko. 
Mikunde > Nyasi > Mikunde Miti > Nyasi.

HATUA ZA KILIMO HIFADHI.
1. Andaa shamba.
* Punguza uchachu wa udongo kama upo kwa Mbolea ya Minjingu, Chokaa au mmea uitwao Lupins.
* Tindua au katua kina kirefu kuondoa Mgandamano wa udongo kama upo.
* Panda Matandazo yasiyooza haraka na yenye mazap au mabaki mengi. Matandazo yanaqeza kupandwa kwa mfumo wa Kilala bora, Mchanganyiko au Kupokezana.
2. Fyeka na laza matandazo kwa Nyengo, Gogo au Kisu Kidekuzi ( Chopping knife roller ) juma 1-2 kabla ya kupanda zao kuu.
3. Pulizia dawa ya kuua wadudu ( kama ni lazima ).
4. Panda kwenye Matandazo kwa Kipanzi maalum. Weka mbolea ya asili ya kupandia.
5. Palilia magugu nachache yatakayoota kwa kung'olea au kupiga dawa ya magugu.
6. Rutubisha kwa kuongeza kiwango cha mbolea za viwandani ( kwa mwaka wa kwanza ). Dhibiti magonjwa/wadudu hasa kwa dawa za asili.
7. Kwa msimu unaofuata, rudia mzunguko kwa kilimo cha mzunguko wa mazao.
MANUFAA YA KILIMO HIFADHI.
i. Kuongeza mboji na rutuba ya udongo. Hatimaye mahitaji ya mbolea za viwandani hupungua.
ii. Kupunguza mahitaji ya nguvu kazi na muda kwa hadi 60%. Hii inatokana na kutohitajika kukatua na haro.
iii. Kuongeza kiwango cha mvua kupenya kwenye ardhi na udongo kutunza unyevunyevu. Athari za vipindi vya ukame au mvua kupita kiasi ni ndogo zaidi katika kilimo cha matandazo.
iv. Kupunguza mmomomonyoko wa udongo. Matone ya mvua hukingwa yasidondoke kwenye udongo n kuusambaratisha. Uchafuzi wa maji katika mito hupungua.
v. Kupunguza gharama za uzalishaji mazao na kuongeza faida. Baadhi ya Matandazo ( Mucuna, Marejea, Desmodium, Vetch ) yana uwezo wa kudhibiti magugu sugu kama ndago.
vi. Kupunguza uchakavu wa zana, mitambo na mafuta kwenye kilimo.
vii. Kutindua na kulainisha ardhi iliyo gandamana. Mizizi ya baadhi ya mimea ya matandazo ( Mbaazi, Fiwi, Nyonyo, Utupa, Marejea pori ) inaweza kwenda chini hadi futi nne.
CHANGAMOTO ZA KILIMO HIFADHI.
. Ni shida kuwashawishi wakulima, wataalam wa ugani, na hata watafiti kubadili mtazamo na kukubali Kilimo Hifadhi.
. Inahitaji kiwango cha juu cha nidhamu na usimamizi wa kilimo.
. Kuzuia uchungaji holela wa mifugo.
. Kuzuia utayarishaji wa mashamba kwa kuchoma moto.
. Matandazo ni makazi salama ya Panya na Nyoka.
Kwa hiyo ndugu zangu wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo, ni vema kuweza kubadili mawazo na mtazamo wa kifikra katika kuongeza kipato kwa gharama nafuu.

No comments:

Post a Comment