Mambo matano ya muhimu kuyafahamu kabla ya kuwekeza kwenye Kilimo - KILIMO NA UFUGAJI

Latest

Karibu uweze kujifunza na kujipatia elimu kuhusiana na kilimo na ufugaji ambapo utajifunza mbinu bora za kilimo na ufugaji pia utajifunza dondoo mbalimbali na mbinu bora na za kisasa za ufugaji

Saturday, October 7, 2017

Mambo matano ya muhimu kuyafahamu kabla ya kuwekeza kwenye Kilimo

Habari ndugu msomaji wa app hii napenda kukaribisha katika  mafunzo ya kilimo yatakayokua yanakujia hapa, lengo ni kuhakikisha unapata elimu na maarifa ya jinsi ya kufanya kilimo chako  kua biashara inayolipa zaidi. hata yule ambaye hayajwahi kulima, kupitia jukwa hili ataweza kujifunza mengi na kua sio mkulima tu, bali mwekezaji kwenye kilimo. 
Leo hii napenda tuanze kujifunze  mambo matano ambayo kila mtu aliye na ndoto ya kuwekeza kwenye kilimo ni lazima ayafahamu vizuri. Kutotilia maanani moja ya mambo haya kunaweza kupelekea ukakichukia kilimo. Leo tutaanza na mambo mawili.
1.       Soko
Hili ndilo jambo la muhimu kwenye kila uwekezaji au kwa maana nyingine biashara yeyote lazima itegemee soko.  Na hapa ndipo wengi wanakosea sana wakulima wadogo na hata vijana wanaoingia kwenye kilimo maana wengi wanazalisha kwa kufuata mkumbo kwa vile wengi wanazalisha wakati huo au amesikia labda kilimo cha zao Fulani kinalipa. Kabla ya kuwekeza kwenye kilimo lazma uanze kwa kulitambua soko lako. Lazima uzalishaji wako uwe unaendeshwa na soko. Unatakiwa kua na taarifa za kutosha kuhusu soko, kujua soko linasemaje, ni wakati gani watu wengi wanakua wamezalisha, wakati gani bidhaa hii inakua kwa wingi sokoni, ni wakati gani inakua hadimu na ni kwanini? Usizalishe kwa vile ni msimu wa kuzalisha kwamba unaona mko wengi. Watu wengi wanaofaidika kwenye kilimo ni wale ambao hawafuati mkumbo kwenye kuzalisha wao wanajua kucheza na wakati, wakati bidhaa ile ni hadimu au wakati ambao sio msimu wa kuzalisha, ndio wakati wa wao kuzalisha na hivyo kupelekea kupata faida nzuri zaidi. Hata kampuni kubwa zinazowekeza kwenye kilimo kwanza wanakua na soko la uhakika, aidha baada ya kufanya utafiti wa kutosha au kwa kuingia mikataba na wateja wao. Vyovyote vile lakini wanchokua na uhakika nacho ni kua wanajua ni wapi watauza baada ya kuzalisha. Mfano kwa kampuni zinazozalisha maua Arusha na maeneo mengine soko lao kubwa liko uholanzi (Amsterdam Auction) na ndio maana asilimia kubwa ya wamiliki wa kampuni hizo ni waholanzi maana wanalijua vizuri soko la maua. Ila kwetu hali ni tofauti badala ya kuanzia sokoni sisi tunaenda moja kwa moja shambani kuzalisha baada ya mazao kukomaa na kua tayari kuvuna ndio tunalikumbuka soko, yaan umeshazalisha ndo unaenda kutafuta soko, bila kujua pengine ulichonacho hakihitajiki na soko.
Wengine wanaweza kusema hatuwezi kuwekeza kwenye kilimo maana soko hakuna, hasa wakulima wadogo wengi wanafahamu soko ni pale kwenye mkusanyiko wa watu wengi kama kwenye minada, magulio au kwenye masoko kama kilombero arusha, mabibo dar n.k.  Unachotakiwa kujua ni kwamba kuna aina kadhaa za masoko mfano masoko ya ndani yasiyo rasmi, masoko ya kitaasisi  kama mahoteli, mashule na mahospitali. Pia kuna masoko ya kiviwanda;  mfano viwanda vya kuongeza thamani kama vya azam au Redgold arusha n.k Bila kusahau masoko ya kimataifa kama ulaya, asia na hata nchi za jirani kama Sudan ambako kumekua na vita na watu wamekua hawana muda wa kuzalisha. Hata hivyo kuna vitu vingi sana vya kujifunza kwenye upande wa soko naona kwa leo tuishie hapa kwa upande wa soko, tukipata muda huko mbeleni tutajadili kwa kina.
2.       Hali ya hewa inayoruhusu kilimo husika
Kila kilimo cha zao fulani kina hali ya hewa au mazingira yanayo kiruhusu kilimo hicho kustawi vizuri. Kwenye eneo hili  tunaangalia maswala ya jotoridi, unyevunyevu kwenye hewa, mvua na sifa za udongo unaosaidia ukuaji wa zao husika. Kuna mazao yanapendelea hali ya joto na kuna mengine yanastawi kwenye hali ya baridi. Mfano kama mananasi yanapendelea ukanda wa joto na ndio maana yana stawi sana ukanda wa pwani huko. Katika sifa za udongo kuna sifa za kikemikali au kifikzikia. Mfano wa sifa hizo ni kama pH ambacho ni kipimo cha kiwango cha asidi na alikali ya udongo. Hii ina maana pH ya udongo wako ikiwa ndogo chini ya 5 udongo wako una kiwango cha asidi  na ikiwa kubwa zaidi ya 8 maana yake udongo wako una kiwango fulani cha alikali. Katika aina ya udongo inakubidi ufahamu ni udongo mfinyanzi, tifutifu au kichanga. Usije ukapanda mpunga kwenye udongo wa kichanga wakati mpunga unapendelea udongo unaotuamisha maji. Au unapanda vitungu kwenye udongo unashikamana sana (mfinyanzi) wakati kitunguu kinahitaji udongo wenye kuachia (tifutifu) ili kiweze kujijenga vizuri. Lakin ngoja nisiingie kwa kina sana hapa kwenye udongo maana kuna mambo mengi sana na ndio maana watu wanasomea shahada za chuo kikuu kwenye masuala ya udongo na hata wengine wanakua maprofesa wa udongo.
Lengo la kukupitisha hapa kidogo ni ili ufahamu kwamba baada ya kupata soko la uhakika na kujua ni zao gani kinachofuata ni kujua maeneo gani zao hilo linastawi, ni udongo wa aina gani unaofaa. Unashauriwa kabla  ya kupanda uchukue sampuli ya udongo ukapime maabara kujua sifa za udongo wa shamba lako. Zipo taasisi za serikali na binafsi zinazotoa huduma ya upimaji udongo. Taasisi hizo ni kama taasisi za utafiti wa kilimo kama SARI (Arusha) ARI Ukiliguru ( Mwanza), ZARI Kizimbani (Zanzibar), ARI Maruku Kagera, ARI Kibaha n.k Pia zipo taasisi za elimu kama Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Mororgoro. Ukishapima udongo unapewa ushauri wa zao gani linaweza kustawi vizuri kwenye shamba lako lakini pia unapata ushauri wa aina gani ya mbolea unatakiwa kutumia. Gharama ya upimaji inategemea na wingi wa vitu unavyotaka kupima kwenye huo udongo.
Kwa kifupi maeneo mengi ya nchi yetu ni mazuri sana kwa kilimo na ndio maana tunaona nchi nyingi zinakuja kuwekeza kwenye kilimo nchini kwetu. Hata hapa kwenye jumuiya ya afrika mashariki wenzetu wanaimezea mate sana ardhi yetu yenye rutuba. Nchi ya Tanzania inauwezo mara kumi ya Kenya au kwa maneno mengine ina hali ya hewa nzuri katika kuzalisha mbogamboga mara kumi zaidi ya Kenya, maeneo mengi ya Kenya ni makame sana. Lakin cha kushangaza wenzetu wanazalisha mazao hayo na kuuza nje ya nchi mara kumi zaidi ya Tanzania.  Je ni kwanini? Basi naomba tukutane tena wiki ijayo hapa hapa

No comments:

Post a Comment