Njia 10 Za Kupunguza Magonjwa Ya Mlipuko Wa Kuku - KILIMO NA UFUGAJI

Latest

Karibu uweze kujifunza na kujipatia elimu kuhusiana na kilimo na ufugaji ambapo utajifunza mbinu bora za kilimo na ufugaji pia utajifunza dondoo mbalimbali na mbinu bora na za kisasa za ufugaji

Friday, November 17, 2017

Njia 10 Za Kupunguza Magonjwa Ya Mlipuko Wa Kuku

Mlipuko wa magonjwa ni moja ya sababu za hasara kubwa kwa wafugaji na vifo vinavyotokea kwa wakati mmoja. Pindi mfugaji anapokumbwa na janga la vifo vya ndege, kabla ya kufikia mwisho wa mzunguko wa uzalishaji hivyo basi asitarajie kupata faida nzuri mara baada ya mauzo.

Hasara itokanayo na vifo inaweza kuepukika au kupunguzwa na kutokea kwa kiasi kidogo. Hili linawezekana, ifuatayo ni namna ya kufanikisha hilo;-

1. Osha vyombo vya maji kila wakati na mwaga maji yaliyobaki.
Hakikisha unamwaga maji yaliyosalia mbali na kuosha chombo na sabuni kila siku, weka maji safi yasiyo na dawa na wala usitumie maji ya mto au yale usiyoyajua chanzo chake. Kama utaweka maji dawa basi tumia ‘vitamini’ muhimu kama ‘vitalyte’ ambazo zinasaidia kuua vijidudu.

2. Wape maji kabla ya chakula.
Ndege wapo tofauti na binadamu au wanyama wengine. Hakikisha unawapa maji kabla ya chakula hasa kama unatumia maranda, hii ni kuhakikisha hawakanyagani wanapogombania chakula sehemu moja.

3. Usiwape chakula chenye uvundo.
Ni hatari sana kuwapa ndege/kuku wako chakula chenye ukungu, ni kama kuwalisha sumu. Ukungu au uvundo huwafanya kuku waugue kirahisi sana au kuwasababishia madhara mengine kiafya.

4. Fuatilia kwa makini ratiba za chanjo na tiba.
Mfugaji unatakiwa kupata tiba na chanjo sahihi kwa ndege unaowafuga. Kuchanja ndege kutasaidia sana kuimarisha kinga yao dhidi ya magonjwa hatari kama kideri, ndui, gumboro na mareksi. Dawa kama vile za minyoo na antibayotiki ni muhimu sana kwenye afya ya kuku na ndege wengine.

5. Nunua na fuga vifaranga wenye afya njema.
Matatizo mengi ya afya ya ndege au kuku ni matokeo  ya maisha duni ya awali ya kuku hao au huwa wanarithi. Itambulike hivi, baadhi ya ndege/kuku hurithi afya mbovu kutoka kwa wazazi wao. Hata hivyo baadhi ya watotoleshaji pia wanafuga kuku ambao wana afya mbovu na hivyo huuza vifaranga au mayai dhaifu na waathirika na hivyo mnunuzi anajikuta ananunua matatizo.

6. Zuia mkusanyiko wa hewa ya ammonia.
Maranda yakikaa muda mrefu bandani, hufanya hewa ya ammonia kuzalishwa kwa wingi, hewa hii hufanya ndege wapaliwe hadi kufa. Kila mara ondoa maranda mabichi au yaliyovunda na weka mengine haraka iwezekanavyo ili kuepuka vifo vitokanavyo na kupaliwa au magonjwa ya mfumo wa hewa.

7. Zuia panya na vicheche.
Banda la ndege linatakiwa lisiruhusu panya au wanyama wadogo jamii ya kicheche kuingia ndani, na ndege wa mwituni kwa kuweka nyavu au kupulizia dawa, ikiwa watapata upenyo wataua na kula ndege/kuku wako na kuacha vimelea vya magonjwa wanapokula vyakula au kunywa maji ya ndege wako.

8. Zingatia usafi na usalama.
Kipengele hiki cha usafi na usalama ni kipana  ila unachotakiwa kufanya ni kuzingatia usafi nje na ndani ya banda. Unatakiwa ukamilishe usalama wa afya ya ndege/kuku wako kila wakati, jambo ambalo wafugaji wengi hutekeleza pindi wanapo shitukizwa na mlipuko wa magonjwa.

9. Wape chakula cha kutosha.
Ndege kama walivyo wanyama wengine, hawawezi kukua na kuzalisha vizuri endapo wanapewa chakula duni na kidogo. Chakula bora ni msingi imara  na ni kinga kwani chakula duni hupelekea uzito kupungua na kinga kuwa chini na hivyo hufa mapema. Jitahidi wape kuku chakula cha kutosha ila usiwazidishie.

10. Wakinge dhidi ya baridi kali.
Baridi kali ni adui kwa afya ya wanyama, ndege na binadamu. Jaribu kila uwezavyo kuwakinga kuwakinga ndege wako na baridi kali kwani inaua haraka sana kama sumu. Wawekee chanzo cha joto wakati wa baridi au jenga banda ambalo halipitishi baridi kali.

Hizo ndizo njia muhimu ambazo ukiwa mfagaji unazoweza kuzitumia ili kukinga magonjwa yanatokanayo na kuku.

No comments:

Post a Comment