UTANGULIZI
Zao la mpunga linazalishwa na nchi zipatazo 40 za Afrika, umuhimu wa zao hili umekuwa ukiongezeka kwa kasi kubwa kuliko mazao mengine ya chakula kwa sasa. Mpunga umechukua nafasi ya pili kwa chakula aina ya nafaka baada ya mahindi, katika nchi nyingine kama zile za kaskazini mwa Afrika mpunga unachukua nafasi ya kwanza. Kwa muktadha huo taasisi za utafiti wa mazao ya kilimo Afrika na Dunia kwa ujumla wameanza kufanya tafiti mbalimbali na kuzalisha aina kadhaa za mbegu bora ya mpunga zinazoweza kupatikana kwa wakulima.
Katika bara la Afrika mpunga unalimwa sana magharibi mwa bara 42%, kaskazini 23%, kati 1.2% na kusini karibu 1%. Nchi zinazolima mpunga ni Benin, Burkina, Cameroon, Demokrasia ya Kongo, Kongo, Chad, Ivory Coast, Gabon, Gambia, Guinea, na Bissau, Madagascar, Mali, Mauritania, Senegal, Togo,Nigeria, Liberia, Sierra Leone, Misri, Tanzania, Kenya, Ruanda na Uganda.
Karibu 75% ya mpunga katika bara la Afrika unazalishwa na wakulima wadogo wanaozalisha wastani wa chini ya tani 2 kwa hekta, kwenye maeneo ya umwagiliaji chini ya 11% ya ardhi inayoliwa barani Afrika.
Ukanda wa Afrika ya Mashariki mpunga unaopatikana ni 58% tu ya mahitaji. Wastani wa mavuno ya mpunga kwa hekta nchini Tanzania ni tani 2.4 Kuna umuhimu wa kupata mbegu itakayowezesha wakulima kupata mpunga wa kutosha na kulingana na matakwa yanayokusudiwa na mkulima kujitosheleza kwa chakula na ziada kuweza kumsaidia kupata mahitaji yake baada ya kuuza.
MBEGU DUNI YA MPUNGA HUSABABISHA MAVUNO HABA
Kinachosababisha wakulima kutopata mavuno mengi kwa kifupi ni matumizi ya mbegu duni zinazotoa mavuno haba, sababu nyingine ni matumizi kidogo ya mbolea, teknolojia duni ya uzalishaji na uhaba wa maji. Kuhusu tatizo hili la mbegu duni inaonekana tatizo hilo limeanza kushughulikiwa kama nilivyotangulia kueleza hapo awali, kuhusu jitihada zinazofanywa na taasisi za utafiti ili kutoa mbegu zinazoweza kumsaidia mkulima kuongeza uzalishaji zinahitajika kupata muunganiko wa taarifa na maarifa ili kukidhi matakwa ya wakulima na kuzikubali kwa kuwa wakulima wamekuwa na matakwa yao ya kuchagua mbegu kwa kuzingatia ladha, harufu na muonekano wake bila kujali kiasi cha mavuno kinachopatikana. Kama kutakuwepo njia za kuwaaminisha na kuwafanya waanze kuzitumia mbegu bora zilizozalishwa na ambazo zinatoa mavuno mengi, zenye ukinzani dhidi ya wadudu na magonjwa, zenye kuvumilia ukame, hali ya hewa, kukomaa haraka, zenye faida za lishe, na kuwa na ubora unaokidhi mahitaji ya soko (mlaji), kuna uwezekano mkubwa wa kuongeza mavuno katika zao hilo na kuwafanya wakulima wajitosheleze kwa chakula na ziada kuweza kuuza na kuongeza kipato kuboresha hali ya uchumi katika familia zao kama wataweza pia kuboresha mbegu zao za asili wanazozotumia sasa.
MBINU ZA KUCHAGUA MBEGU BORA YA MPUNGA SHAMBANI
Mkulima, Afisa Ugani na wadau wengine wa kilimo kwa kuzingatia muongozo huu mfupi wataweza kuboresha mbegu hasa zile ambazo zinaonekana kuanza kuchanganyika na mbegu nyingine na kupoteza sifa zake za awali kwa kuzingatia hatua zifuatazo:
Chagua moja au baadhi ya mbegu ulizonazo unazotaka kuziboresha wewe mwenyewe kwa kuzingatia mwongozo ufuatavyo:
· Mbegu ikisha chaguliwa katika msimu wa kwanza ipandwe tena na utaratibu wa kutunza mbegu uliotumka mara ya kwanza ufuatwe katika hatua zote kama inavyoelezwa katika jedwali hapo chini.
· Mbegu itatambuliwa kuwa ni bora nakuthibitishwa baada ya kupitia hatua za kuchaguliwa na kupandwa kwa misimu mitatu hadi minne mfululizo kwa kuzingatia hatua na vigezo vilivyotajwa hapo chini.
· Mkulima na wa wadau wa mbegu wataipitisha mbegu yao kuwa ni nzuri na kuithibitisha pale watakapo ridhika na muonekano wake na ufanisi waliokuwa wanatarajia kutoka katika mbegu hiyo, mfano uotaji na uchanuaji wa sawia, mashine manene na imara, wingi na ujazo wa masuke, ukomaaji wa sawia, upungufu wa mapepe, rangi na umbo zuri la punje uliosawa, mimea na mazao yasiyo shambuliwa na magonjwa.
VIGEZO NA HATUA ZA KUFUATA KUPATA MBEGU ILIYOTHIBITISHWA NGAZI YA WAKULIMA AU JAMII
NB: uchaguzi wa mbegu shambani ubora uzingatiwe hasa katika siku ya 100 hadi 120.
Uchaguzi wa mbegu wakati wa kuvuna na kwenye ghala, uanze wakati wa kuvuna, kuanika, kupembua hadi kuhifadhi.
|
UCHAGUZI WA MBEGU YENYE VIGEZO VYA MBEGU ILIYOTHIBITISHWA
|
|||
GHALANI AU KABLA YA KUPANDA
|
SHAMBANI WAKATI WA UZALISHAJI
|
|||
TABIA
|
UAMUZI
|
TABIA
|
UAMUZI
|
|
Ya miezi 3 hadi 6
|
Itenge inafaa
|
Fupi kuliko nyingine
|
Ing’olewe hima
|
|
Ya zaidi ya miezi 6
|
Usiitumie
|
Ndefu kuliko nyingine
|
Ing’olewe hima
|
|
Yenye ukungu
|
Usiitumie
|
Nyembamba mno
|
Ing’olewe hima
|
|
Rangi mchanganyiko
|
Usiitumie
|
Nene kupita kiasi
|
Ing’olewe hima
|
|
Umbo mbalimbali
|
Usiitumie
|
Majani membamba
|
Ing’olewe hima
|
|
Iliyo vunjika vunjika
|
Usiitumie
|
Majani mapana sana
|
Ing’olewe hima
|
|
Inayonukia
|
Itenge, nzuri
|
Inayonukia
|
Iache iote shambani
|
|
Yenye uzito mkubwa
|
Itenge, “
|
Yenye masuke mengi
|
Iache iote shambani
|
|
Yenye punje nyeupe
|
Itenge, “
|
Yenye masuke imara
|
Iache iote shambani
|
|
Punje zilizojaa
|
Itenge, “
|
Majani mafupi, wima
|
Iache iote shambani
|
|
Iliyokauka vizuri
|
Itenge, “
|
Isiyoathirika na jua
|
Iache iote shambani
|
|
Isiyo na mapepe
|
Itenge, “
|
inayokubali mazingira
|
Iache iote shambani
|
|
Isiyochanganyika
|
Itenge, “
|
inayoota sawa na zote
|
Iache iote shambani
|
|
Isiyo na ugonjwa
|
Itenge, “
|
Isiyoathirika/ ugonjwa
|
Iache iote shambani
|
|
Isiyo na wadudu
|
Itenge, “
|
Isiyoathirika/ wadudu
|
Iache iote shambani
|
MBEGU ILIYOTHIBITISHWA
Itakuwa ni ile iliyochaguliwa na kutengenezwa na wakulima wenyewe kwa kuzingatia mwenendo wa zao hilo shambani katika kila hatua ya uotaji. Mbegu hiyo itakuwa ni ile iliyobaki baada ya kuondolewa makando na kasoro zinazoweza kuathiri ufanisi wa mbegu mfano mbegu dhaifu, zilizodumaa, zilizoshambuliwa na magonjwa na wadudu, zinazo refuka kuliko zingine, zilizofupi kuliko zingine, zenye rangi tofauti, zenye maumbo na tabia tofauti na tabia za jumla za zao husika la mpunga.
Mbegu itathibitishwa na wakulima kuwa ni bora endapo itarejea sifa yake ya awali kama kuwa na uotaji unaolingana, kufanana kwa kila hali, rangi, umbo, ladha na harufu nzuri, uzao mkubwa, uimara wa suke na ukinzani idhidi ya magonjwa, ukame, hali ya hewa nk.
NB;
Uthibitisho huo hautawahusu wakulima wengine wasiohusika na mchakato wa kuthibitisha mbegu hiyo na wala wakulima waliohusika hawatakuwa na dhamana ya kudai haki ya kuwa watengenezaji wa mbegu hiyo, wakulima wengine wanaweza kuitumia mbegu hiyo na kukubaliana na matokeo na ufanisi wa mbegu hiyo kulingana na maelezo ya wakulima waliohusika na mchakato wakuthibitisha mbegu hiyo.
Aidha, mbegu hiyo haitahusishwa na mbegu nyingine zinazo zalishwa kwa kuzingatia hatua za kisayansi. (seed breeding, varietal seed selection, etc) bali ichukuliwe kama njia ya kuboresha mbegu ya wakulima wa eneo hilo tu, (Improving seed quality).
Nawatakia kilimo chema chenye tija na kinachotosheleza haja zenu,. Tunaweza kuwasiliana kwenye mtandao kwa kutumia nywila iliyopo hapo chini. Ahsante sana!
Makala hii imeandikwa na kuandaliwa na
Gift Mayagila.
Mto wa Mbu, Monduli- Arusha.
Giftgogo70@yahoo.com
Imeletwa kwenu na mtandao ulio jikita katika kusaidia wakulima na wafugaji wadogo wadogo
IMANI LUBABA
rubabaimani@gmail.com
+255764148221Usiache kutembele Channel yetu, ili kupata elimu zaidi kwa kubofya picha juu, na pia subscribe ili kua karibu nasi zaidi.
na unaweza kujiunga na blog yetu
USISAHAU KUPAKUA / KUDOWNLOAD APPLICATION YA KILIMO BORA IPO PLAY STORE ILI UPATE HABARI KWA URAHISI BONYEZA LINK HII KUDOWNLOAD ==> https://ift.tt/2tqvrGF
No comments:
Post a Comment