MAGONJWA YA NG'OMBE. - KILIMO NA UFUGAJI

Latest

Karibu uweze kujifunza na kujipatia elimu kuhusiana na kilimo na ufugaji ambapo utajifunza mbinu bora za kilimo na ufugaji pia utajifunza dondoo mbalimbali na mbinu bora na za kisasa za ufugaji

Friday, October 5, 2018

MAGONJWA YA NG'OMBE.

Ndugu wakulima na wasomaji wangu kwa ujumla, leo napenda tujulishane na kukumbushana kuhusu baadhi ya magonjwa ya ng'ombe. Leo tutaangalia na kujadili magonjwa mawili hivi. 

I. MINYOO YA NG'OMBE. 

Ugonjwa wa minyoo husababisha hasara kwa mfugaji wa ng'ombe . Utafiti unaonyesha kuwa ng'ombe wengi wanaathirika na minyoo hiyo hupunguza uzalishaji. Aidha utafiti unaonyesha kuwa tatizo la minyoo kwa ng'ombe limeenea hapa nchini kwetu. 

(i) AINA ZA MINYOO. 

Minyoo inayoathiri ng'ombe imegawanyika katika makundi mbalimbali kama ifuatavyo; 

- Minyoo inayoishia kwenye maini ya ng'ombe (liverflukes). 

- Minyoo inayoishia kwenye mapafu (lungworms). 

- Minyoo mikubwa ya mviringo (large roundworms). 

- Minyoo midogo ya mviringo (small roundworms). 

(ii) MZUNGUKO WA MAAMBUKIZI. 

Minyoo hupitia njia zifuatazo: 

- Mnyama kuambukizwa na mwingine. 

-Kupenya kwenye ngozi ya ng'ombe. 

- Ndama kupata minyoo kupitia kwa mama (ng'ombe) alieathirika kwa minyoo wakati wa kuzaliwa. 

- Ng'ombe kula mayai ya minyoo yaliyomo kwenye majani wakati wa malisho. 

- Ndama kupata minyoo wakati wa kunyonya maziwa ya ng'ombe aliyeathirika. 

(iii) DALILI ZA NG'OMBE ALIYEAMBUKIZWA. 

- Kupoteza uzito 
- Kukosa hamu ya kula 
- Kuhara 
- Kupungukiwa na damu 
- Kuwa na homa 
- Afya yake kufifia na hatimaye kufa 
- Tumbo kuwa kubwa kupita kiasi (ndama). 

(iv) TIBA 

Wanyama wapewe dawa za kutibu minyoo mara kwa mara. 
Mfano: 
. NILZAN 
. NILVERM 
. PIPERAZINE 
. ANACUR 
. THIABENDAZOLE 
. YOMESAN 
. OXYDOZIDENE 


(v) JINSI YA KUZUIA MAAMBUKIZI NA KUZUIA MINYOO ISIENEE. 

Minyoo hukingwa kwa njia zifuatazo: 

. Kuepuka kulisha ng'ombe kwenye majani yenye mayai ya minyoo. 

. Ng'ombe wote wagonjwa watibiwe. 

. Epuka kulisha na kunywesha kwenye mabwawa. 

. Usafi wa banda uzingatiwe. 

. Ng'ombe wasiruhusiwe kukanyaga malisho yao hasa kwenye zero grazing. 

(vi) MADHARA YA MINYOO 

. Husababisha upungufu wa damu. 

. Husababisha upungufu wa maziwa. 

. Ng'ombe huweza kufa. 


II. UGONJWA WA MAPELE NGOZI 

Mapele ngozi ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyojulikana kama Capripoxvirus. Virusi hivi huweza kukaa kwenye ngozi iliyokauka hadi siku 18. 

Ugonjwa huu huwapata ng'ombe wa umri wowote, aidha virusi hivi hufa kwa muda mfupi katika kemikali mbalimbali kama ether 20% chloroform, farmalin 1% na phenol 2%. 

A. JINSI MAPELE YANAVYOAMBUKIZWA. 

Virusi vya mapele ngozi hupatikana kwenye mapele, mate na majimaji mengine ya mnyama mgonjwa. Ugonjwa huu unaambukizwa kwa kuumwa na mbu jamii ya Andes Culex baada ya kumuuma mnyama mwenye virusi. 

B. DALILI ZA MAPELE NGOZI 

Homa kali ambayo inaambatana na kutokea kwa mapele katika ngozi. Mapele haya yanaweza kuwa na ukubwa wa sentimeta 1 hadi 7 na huonekana katika sehemu ya kichwa, shingo, kiwele na miguuni. Mapele haya hukauka, kunyofoka na kuacha vidonda ambavyo huweza kushambuliwa na bakteria. 

Mapele haya yanaweza pia kutokea katika mdomo. Dalili nyingine ni homa kali ya nyuzi joto sentigredi 40-41.5, mnyama hukosa hamu ya kula, kutoa machozi, kutokwa na makamasi mazito, kuvimba matezi, kupunguza uzalishaji maziwa na kutupa mimba. Baadae mapele hutokea mwili mzima. 

C. JINSI YA KUZUIA MAPELE NGOZI. 

Mapele ngozi unazuilika kwa kuchanja ng'ombe na kurudia chanjo mara moja kila mwaka ili kuongeza nguvu ya kinga. Zingatia kanuni zifuatazo: 

. Ogesha mifugo kwa kutumia dawa ambazo zinaua wadudu ikiwa ni pamoja na mbu wanaoeneza magonjwa ya mifugo. 

. Hamasisha wafugaji wengine kuchanja dhidi ya mapele ngozi na magonjwa mengine ya mifugo kama vile homa ya mapafu, ugonjwa wa miguu na midomo na ndigana kali. 

. Toa taarifa kwa mganga wa mifugo aliyekaribu nawe unapoona dalili za ugonjwa huu ili hatua zinazopaswa zichukuliwe. 

. Tenga wanyama wagonjwa na kuwapatia matibabu ya vidonda. 

. Nunua ng'ombe kutoka eneo ambalo halina ugonjwa. 

Kwa leo hebu tukomee hapa na tuweze kuhudumia mifugo yetu kwa ueasaha. 

Ahsanteni! 

No comments:

Post a Comment