KANUNI ZA MSINGI ZA UJENZI WA MABANDA YA KUKU WA NYAMA
KUKU 1,000 - 10,000 (UFUGAJI WA KIWANGO CHA KATI) ...mwendelezo...
[[ Kwa wajasiliamilia wenye mtazamo wa kufanya uwekezaji mkubwa. Mtazamo wa kiviwanda.
Kuwa na uwezo wa kusambaza kuku bora kwa idadi kubwa katika mwaka mzima!
Ufugaji wa kati kitaalamu wenye lengo la kukua kwenda kiwango cha juu (kuku zaidi ya 100,000/=)
Uhitaji wa kuku kwa Dar es Salaam na mikoa mingine ni mkubwa, hasa kuku wa kiwango cha ubora!
Hii ni kwa wale tu wenye maono na wenye kujitoa kwa dhati! Fursa ni yako mpaka soko la kimataifa! ]]
MAMBO YA MSINGI KATIKA SHAMBA LA KUKU
=== Uchaguzi wa shamba
-- Weka shamba sehemu ambayo inaruhusiwa kisheria kwajili ya ufugaji (Ofisi za ardhi halmashauri zitakusaidia)
-- Nunua shamba kwa kufuata taratibu za kisheria na uwe na umiliki halali wa kisheria
-- Hakikisha shamba lako ni kubwa la kutosha huku ukizingatia upanuzi wa siku za mbeleni
-- Chagua eneo ambalo jumla ya gharama za uzalishaji zitakuwa ndogo zaidi (malighafi na wafanyakazi)
-- Ni vyema sana shamba lako liwe jirani na soko ili kupunguza gharama za usafiri
-- Chagua eneo ambalo malighafi za uzalishaji zinapatikana (maji, chakula…)
-- Ni vyema shamba lako liwe sehemu ambayo maji hayatuami, kama si hivyo basi uboreshaji wa kitaalamu ardhi ufanyike
-- Shamba liwe katika sehemu ambayo mabanda yataweza kupata hewa nzuri na safi
-- Ni vyema shamba lako liwe mbali na makazi na shughuli za watu
-- Chagua eneo ambalo litakuwa na ulinzi na usalama (maeneo ambayo hayana migogoro, vibaka…)
-- Hakikisha kuwa shambani mwako umeweka mifumo ya kudhibiti majanga ya moto
=== Maboresho ya shamba
-- Dhibiti mmomonyoko wa ardhi kwa njia stahiki
-- Hakikisha kuwa eneo lako lipo juu ya kiwango cha maji ya mafuriko ya eneo hilo
-- Yatengenezee maji mtiririko mzuri ili yasituame na uyaelekezee katika njia inayofaa
-- Kama eneo linatuamisha maji, basi waweza kulinyanyua juu kwa mawe na kifusi
-- Panda ukoka na boresha mandhari iwe ya kupendeza
-- Upande ambao utakuwa una mwonekano mbaya, waweza kupanda miti ili kuukinga
-- Hakikisha kuwa shamba lako limezungukwa kwa usalama wa kutosha
-- Ni vyema shamba lako likiwa na wigo uliozunguka pande zote na geti la kuingilia
-- Wigo wako uwe imara kuhakikisha kuwa wanyama hawachimbi chini na kupita
-- Tengeneza barabara ya kuingilia inayotosha katika kiwango cha kitaalamu huku ukifuata taratibu na sheria
-- Ondoa vichaka, fukia mashimo hatarishi ya eneo hilo n.k
-- Ondoa vishawishi vyote vya mwewe, nyoka n.k.
-- Dhibiti wanyama kama nyoka, mwewe na jamii hiyo
=== Mpangilio wa ndani wa shamba
-- Kuwa na shamba kubwa la kutosha shughuli zote huku ukizingatia upanuzi wa siku za mbeleni
-- Fahamu idadi ya kuku utakao fuga huku ukizingatia upanuzi wa baadaye
-- Idadi ya mabanda, aina ya nyumba zitakazo hitajika zitategemea idadi ya kuku na namna ya mfumo wa kuendesha mradi wako
-- Shamba lipangiliwe kwa namna ambayo kutakuwa na mtiririko mzuri wa shughuli na nafasi ya kutosha
-- Mpangilio wa shamba uruhusu nafasi ya kupita vifaa kati ya banda moja na jingine
-- Hakikisha kuwa mabanda yamekaa kwa namna na nafasi ambavyo magonjwa hayataweza kusafiri toka banda moja kwenda jingine
-- Mabanda yatazame upande ambao utahakikisha kuwa kipindi cha joto hewa na upepo mzuri unaweza kuingia na kupooza
-- Mabanda yakae upande ambao ni huru na viatalishi kama magonjwa, shughuli za binadamu n.k.
-- Hakikisha kuwa shamba lako limepangiliwa kwa namna ambayo magari yataweza kugeuka na kukata kona
-- Eneo la kutupa taka liwe upande ambao halitaathiri afya ya binadamu na kuku
-- Hakikisha kuwa utupaji taka na utumiaji madawa hauathiri vyanzo vya maji, ardhi na mazingira kwa ujumla
-- Dhibiti harufu na kelele shambani mwako ili zisiathiri majirani
-- Baadhi ya kazi zifanyike muda mzuri ambao hautaathiri majirani
-- Shughuli za binadamu zisiathiri afya ya kuku
-- Baadhi ya nyumba utakazo hitaji ni mabanda ya kuku, mabanda ya kuku wagonjwa, mabanda ya kuku wapya, stoo ya chakula, stoo ya vifaa vya kufanyia kazi, karakana, maabara, ofisi, nyumba ya kulala wafanyakazi na meneja, jiko, vyoo, sehemu ya kuhifadhi magari, banda la kuweka lita iliyokwisha tumika, sehemu ya kudhibiti mizoga ya kuku, sehemu ya kuweka matanki ya maji n.k
-- Hakikisha mradi wako unajitegemea humo humo bila kuhitaji vitu vingi kutoka nje ili kupunguza gharama za uzalishaji na vihatarishi
=== vipimo, umbo na msingi wa banda
-- banda lenye umbo la mstatili ndilo ambalo mara nyingi hutumika sana
-- ukubwa wa banda unategemea idadi ya kuku na shughuli ambazo zitakuwa zinafanyika ndani
-- kwa kuku wa nyama, mita moja ya mraba wanakaa wastani wa kuku 10
-- msingi wa banda unapaswa kuwa imara kubeba uzito wa banda
-- aina ya msingi ujengwe kutegemea na ushauri wa Mhandisi husika
-- piga dawa ya wadudu kwenye msingi kuzuia mchwa na wadudu wengine
-- zuia unyevu kuja sakafuni kwa kutumia DPM
- sakafu ya banda iwe ya zege kuhakikisha uimara, ugumu na kuzuia zaidi unyevu
--hakikisha msingi umenyoka na pima maji
-- kinga msingi na mmomonyoko wa ardhi
-- kama banda litajengwa kwa nguzo, basi hakikisha zimewekwa na kushikwa vizuri katika msingi
=== kuta, madirisha, milango, paa
-- kutegemea na aina ya kuta utakayotumia, hakikisha imejengwa sehemu stahiki, imara kuhimili mizigo yote
-- kimo cha kuta kiwe chenye kuruhusu shughuli kufanyika ndani ya banda na chenye kuruhusu mzunguko mzuri wa hewa
-- ndani ya banda kuta ziwe laini ili ndege wasijiumize
-- hakikisha kuta zinakiwango cha kutosha cha mpitisho wa joto
-- hakikisha kuta zinauwezo wa kuzuia unyevu
-- weka milango kulingana na uhitaji huku ukizingatia kutoathiri shughuli za banda huku ukihakikisha uimara, ulinzi na usalama
-- weka madirisha yenye ukubwa wa kutosha yenye kuwezesha upepo kupita juu ya kuku
-- tumia nyavu zinazostahili katika madirisha kuweka usalama, ulinzi na udhibiti unaostahili
-- funika madirisha na mapazia maalumu yenye mfumo wa kufunika na kufunga dirisha ili kuruhusu kiasi maalumu cha upepo kupita
-- mapazia yawe yenye kufunika vizuri kuzuia kabisa upepo usiostahiri kupita
-- weka vidirisha vya kupitisha upepo juu mwisho wa kuta kuruhusu upepo wa baridi kuingia ndani kulingana na usanifu wa kitaalamu
-- paa liwekwe lililo imara na kuhimili mzigo
-- ni vyema zaidi upana wa jengo uwe huru bila kizuizi katikati
-- ulalo wa paa uwe mzuri kuruhusu kumwaga maji na kubeba mzigo
-- paa lishikishwe vizuri katika nguzo/ukuta kuhakikisha usalama
-- paa liwe na kiwango maalumu cha mpitisho wa joto
-- paa liweze kuzuia unyevu
-- paa lipitilize nje zaidi ya kuta kuzuia maji ya mvua na jua kuingia ndani ya banda
-- kwa mabanda yaliyo mapana zaidi ya mita 8, madirisha ya kupitisha na kupooza hewa juu paani ni ya muhimu
-- madirisha ya juu paani yafunikwe vizuri kuhakikisha kuwa wadudu, ndege, wanyama na maji hayapiti
-- banda linaweza kuwa na vyumba vya ndani kulingana na uhitaji
-- hakikisha kuwa jengo zima ni imara
-- jengo lote liwe zuri na lenye kuvutia ndani na nje
-- jengo liwe limesanifiwa kuruhusu mzunguko mzuri wa hewa
No comments:
Post a Comment