Vigezo vya uchaguzi wa mayai yanayoandaliwa kwa ajili ya kutotoleshwa
Si kila yai linalotagwa na kuku basi linakidhi sifa na vigezo vya kutotoleshwa ni wazi kuwa kama yai halikidhi vigezo vya kutotoleshwa na kuwa kifaranga hata uwezekano wa kutototoleshwa wenyewe unakuwa haupo. Wafugaji wengi tumekuwa tukikusanya mayai hovyo hovyo na kuyapelekwa kutotoleshwa bila kuzingatia vigezo hivi muhimu;-
1. A) YAWE YAMERUTUBISHWA NA JOGOO
Sifa kuu na muhimu ya utotoleshwaji wa mayai ni kuwa ni lazima yawe yamerutubishwa na jogoo kwa uwiano stahili wa majogoo na mitetea na uwiano unaopendekekzwa ni wa mitetea nane kwa jogoo mmoja.
1. B) YAWE NA GANDA SAFI LISILO NA UFA
Mayai yanayoandaliwa kwa ajili ya kutotoleshwa ni lazima yawe na ganda safi lisilo na uchafu uliogandia.Usafi wa mayai unategemea pia na usafi wa bandani na mahali ambapo kuku wanatagia. Iwapo kuku watakua na miguu misafi na wanataga kwenye viota visafi na ukusanyaji wa mayai unafanywa kwa wakati na kuwekwa kwenye chombo kisafi ni wazi hata mayai yatakuwa safi kabisa na salama tofauti na vinginevyo.
1. C) YAWE NA UKUBWA, MAUMBO NA RANGI ZINAZOWIANA
Mayai yanayoweza kukupa matokeo sahihi ni yale yaliyo na ukubwa unaowiana, maumbo yanayofannana na rangi zinazo fanana usichukue mayai yenye ganda lenye vinundunundu, yaliyo na shape isiyoeleweka, yenye viini viwili au mayai yenye nyufa. Yawe na uzito unaopendekezwa wa 50g-70g. Kutokana na ukweli kuwa mayai madogo yanatotolewa mapema kuliko makubwa ni wazi kuwa mayai madogo yaanze kuatamishwa masaa 8-18 baada ya mayai makubwa kuanza kuatamiwa.
1. D) YASIWE YAMEHIFADHIWA ZAIDI YA SIKU SABA TANGU KUKUSANYWA.
Ili kupata utotoleshwaji wenye tija ni lazima mayai yanayototoreshwa na kuwekwa kwenye mashine yawe yamehifadhiwa kwa kipindi kisichozidi siku saba kabla ya kuanza kuatamiwa.
1. E) YAHIFADHIWE SEHEMU YENYE JOTO STAHILI NA KIASI
Mayai yanayoandaliwa kwa ajili ya kuatamishwa ni lazima yahifadhiwe kwenye chumba kisichopitisha upepo mkali na chenye nyuzi joto 12.8 sentigredi na 15.6 sentigredi na unyevuunyevu wa asilimia 75 hadi asilimia 80.
1. F) YAKUSANYWE SEHEMU YENYE NCHA KALI IKIANGALIA CHINI
Kipindi cha ukusanyaji wa mayai, mayai ni lazima yakusanywe sehemu iliyochongoka ikiangalia chini,mayai yayiyohifadhiwa kwa namna hii hayahitaji kugeuzwa geuzwa.
Uatamishaji wa mayai huweza kufanywa kwa kutumia njia mbili yaani kwa kutumia kuku wazazi kuweza kuyalalia mayai au kwa kutumia mashine inafahamika kama incubator.
MUDA WA UTOTOAJI WA MAYAI KWA NDEGE WA AINA MBALI MBALI
AINA YA NDEGE MUDA WA UTOTOAJI
KUKU SIKU 21
BATA MZINGA SIKU 28
KANGA SIKU 28
BATA MAJI SIKU 28
BATA BUKINI SIKU 28-32
KWARE SIKU 18
UATAMISHAJI NA UTOTOLESHAJI WA MAYAI KWA KUTUMIA MASHINE MAALUM (INCUBATOR).
Uatamishaji wa mayai kwa kutumia mashine maalumu hufanywa kwa kifaa maalum ambacho hujulikana kama incubator. Incubator zipo za aina mbalimbali na ukubwa tofauti tofauti kulingana na mahitaji ya mfugaji. Kifaa hiki ni muhimu kwa mfugaji ili kuweza kuzalisha vifaranga vyenye ubora. Incubator ni vyema ikatumiwa kwa kuzingatia masharti maalum ili kuweza kupata matokeo yenye tija iwapo kama kifaa hiki hakitosimamiwa ipasavyo huweza kuwa chanzo kimojawapo cha maradhi sugu kwa kifaranga.
MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE UATAMISHAJI WA MAYAI KWA KUTUMIA MASHINE:
1. A) KIASI CHA JOTO
Mayai yanayototoleshwa kwenye mashine huifadhiwa kwa kiwango maalumu cha joto kinachozalishwa na mashine kiasi cha 25-30 BC. Ukuaji wa kiini tete (embryo) hutegemea kiwango maalum cha joto iwapo kiwango kicho cha joto hakitozingatiwa ni wazi hata kiasi cha mayai yatakayototoleshwa hakitoridhisha kutokana na viini tete vingi kufa.
1. B) KIASI CHA UNYEVU UNYEVU NDANI YA MASHINE
Kipindi cha uatamiaji, mayai hupoteza 11-12% ya uzito wake kutokana na kupoteza unyevu. Kiasi cha unyevu kwenye incubator ndicho kinachosaidia kuweka sawa uwiano wa unyevu kwenye mayai. Upotevu mkubwa wa kiwango cha unyevu kwenye mayai katika hatua za mwazo za ukuaji hupelekea kiini tete kufa na hatimaye yai kuharibika.
1. C) KIASI CHA HEWA KINACHOINGIA NA KUTOKA NDANI YA MASHINE
Kiasi cha unyevu, hewa (oksijeni na carbondioxide) kinachoingia na kutoka ndani ya mashine ni jambo la muhimu kabisa, hii ni kutokana na ukweli kwamba kiini tete kinachokua huhitaji hewa ya oksijeni na kutoa carbondioxide na unyevu hiyo kiasi cha unyevu na carbondioxide kisipo ruhusiwa ipasavyo huweza kusababisha kufa kwa kiini tete.
D)NAMNA MAYAI YALIVYOKAA NA KUGEUZWA KWENYE MASHINE
Ili kupata utotoleshaji wenye tija ni wazi lazima mayai yawe yanageuzwa kwa namna ambayo hayatoruhusu kiini tete kushikana na ganda la yai, ugeuzwaji wa mayai kwa kutumia mikono kwenye incubator ndogo ni lazima ufanywe kwa kuhakikisha mikono inakuwa misafi ili kuzuia bacteria kuingia kwenye yai.
1. E) UCHAGUZI NA UHIFADHI SAHIHI WA MAYAI BORA
Ili kupata matokeo bora ya kifaranga ni lazima mfugaji azingatie upatikanaji wa mayai yaliyo bora yaliyotagwa na kuku mzazi mwenye afya na yaliyorutubishwa na jogoo lenye afya na linalofaa kwa mbegu. Ifahamike pia si kila yai linalotagwa na kuku linafaa kutoa kifaranga chenye ubora.
1. F) USAFI
Mayai kwa ajili ya kutotolesha vifaranga vyenye ubora ni lazima yawe masafi, yamekusanywa na kuhifadhiwa kwenye vyombo visafi na yatakayowekwa kwenye incubator safi iliyo kwenye chumba kisafi. Usafi ni jambo la muhimu sana kwenye kupata kifaranga chenye ubora na kisicho na maambukizi yoyote ya bakteria.
1. G) KUNYUNYIZA DAWA ZA KUUA WADUDU KWA USAHIHI
Mashine ya kutotolesha mayai inapaswa kusafishwa kwa dawa maalum mara kwa mara ili kuzuia kuzaliana na kukua kwa bakteria kwa kiwango kikubwa. Dawa hizi ni lazima zinyunyizwe kwa usahihi kabisa ili kufanya kazi inavyostahili.
1. H) UWEPO WA HEWA YENYE HARUFU NDANI YA MASHINE
Kama kuta za ndani za incubator zimepakwa rangi tunashauri pia mfugaji aweze kujiridhisha na kiwango cha harufu ya rangi inayotoka na madhara yake kwa kiini tete.
Tembela blog hii kila siku
"""""""""""""""""""
No comments:
Post a Comment