UFUGAJI: Jifunze namna ya Kutengeneza Madawa ya Asili yatokanayo na Mimea yanayosaidia katika Tiba na Kinga za Maradhi mbalimbali ya Kuku - KILIMO NA UFUGAJI

Latest

Karibu uweze kujifunza na kujipatia elimu kuhusiana na kilimo na ufugaji ambapo utajifunza mbinu bora za kilimo na ufugaji pia utajifunza dondoo mbalimbali na mbinu bora na za kisasa za ufugaji

Monday, March 13, 2017

UFUGAJI: Jifunze namna ya Kutengeneza Madawa ya Asili yatokanayo na Mimea yanayosaidia katika Tiba na Kinga za Maradhi mbalimbali ya Kuku


Leo katika makala hii tutaangalia namna ya kuweza kutumia sehemu mbalimbali za mimea yetu kutengeneza dawa kwa ajili ya kutubu magonjwa mbalimbali yanayokumba mifugo yetu hususani
kuku, Makala hii nimeiandaa kutokana na changamoto nyingi ambazo zinawakumba wafugaji wengi hapa nchini hususan wale wasiokua na mitaji ya kutosha, Hivyo kupitia makala hii utajifunza njia rahisi na bora ya kupambana na magonjwa mbalimbali yanayokumba mifugo yako.

A.  Sehemu za mimea zinaweza kuwa: Majani, Magome, Mbegu, Maua au Matunda

B.  Umuhimu wa kutumia tiba zenye asili ya mimea:

•  Hupatikana kwa urahisi.
•  Ni rahisi kutumia.
•  Gharama nafuu.
•  Zinatibu vizuri.
•  Hazina madhara.

C.  Baadhi ya Mimea inayotibu Maradhi ya Kuku:

1.  Mwarobaini (Majani, Mizizi, Magome):
Hutibu magonjwa yafuatayo:
•  Typhoid.
•  Kuzuia Kideri.
•  Kuhara.
•  Mafua. 
•  Vidonda.

2.  Shubiri Mwitu (Aloe vera):
Chukua majani 3-5 makubwa, katakata na loweka ndani ya maji lita 10 kwa masaa 12 hadi 16. Wape kuku kwa siku 5 - 7.
Isiyotumika mwaga na tengeneza nyingine baada ya masaa 12.

Mchanganyiko huu unaweza kutibu:
•  Kideri/Mdondo (Mdonde/Chikwemba/Kitoga/Chinoya/Sotoka)
- inyweshwe kabla kwa kinga.
•  Homa ya matumbo (Typhoid).
•  Mafua (Coryza).
•  Kipindupindu cha kuku (Fowl Cholera). 

3. Mtakalang’onyo (Euphorbia):

Chukua Majani makubwa 3-5, ponda, weka katika lita 10 za maji kwa masaa 12-16, chuja na wape kuku. Isiyotumika mwaga na tengeneza nyingine.

Mtakalang’onyo hutibu:
•  Kideri/Mdondo (Mdonde/Chikwemba) - inyweshwe kabla kuzuia
•  Gumboro.
•  Ndui.
•  Kuhara damu (Coccidiosis).

4.  Mbarika (Nyonyo):
Hutibu Uvimbe.

Weka majani ya mbarika ndani ya majani ya mgomba kisha weka ndani ya jivu la moto, kisha kanda sehemu yenye uvimbe kwa kutumia majani hayo ya mbarika.

5.  Mlonge (Mlonje):
Ina vitamini A na C. 

Chukua majani ujazo wa mikono miwili (gao mbili). Kisha yapondeponde na kuyaweka katika lita 10 za maji na iache kwa masaa 12-16, chuja na wape kuku. Isiyotumika mwaga na tengeneza nyingine. 

Mlonge hutibu:
•  Mafua.
•  Kideri - inyweshwe kabla kwa kukinga
•  Kipindupindu cha kuku (Fowl Cholera).
•  Homa ya matumbo
•  Ini.

6.  Konfrei:
•  Ina madini na vitamini nyingi.
•  Hutibu vidonda na majipu.

7.  Ndulele (Dungurusi, Makonde, Tura/Ndula):
•  Majani hutibu Minyoo.
•  Matunda hutibu Vidonda.

8.  Papai (Majani):
Chemsha magao mawili ndani ya maji lita 6 hadi ubakie na lita 1. Poza kisha chuja. 
Hutibu: Minyoo

9.  Mwembe:
Majani magao mawili, ponda na chemsha ndani ya lita 6 za maji hadi ibaki lita 1. Wape kwa siku moja.

Mwembe hutibu:
•  Homa ya matumbo.
•  Mafua.
•  Kinga ya Kideri/Mdondo.

10. Mpira:
Chemsha majani au mizizi.

Mpira hutibu:
•  Tumbo
•  Vidonda na majipu

11.  Minyaa (Cactus):
Hii ni aina yenye majani manene-hadi kufikia nusu nchi na mapana hadi kufikia upana wa viganja viwili vya mikono. 

Minyaa hutibu: (Angalia inaunguza au kubabua).
•  Vidonda.
•  Ngozi.
•  Uzazi.

12. Pilipili Kichaa:
Pondaponda kiasi kisha changanya na maji na wawekee kuku wawe wanakunywa kwa muda wao. Inasemekana inasaidia kutibu Mdonde (lakini mapema kabla maradhi kuingia).

Kwa maoni na ushauri tafadhali tuandikie kwenye kisanduku cha maoni hapo chini na tutakujibu.

Ahsante kwa kutembelea mtandao wetu

No comments:

Post a Comment