FURSA KUPITIA TEKNOLOJIA YA KILIMO CHA GREENHOUSE - KILIMO NA UFUGAJI

Latest

Karibu uweze kujifunza na kujipatia elimu kuhusiana na kilimo na ufugaji ambapo utajifunza mbinu bora za kilimo na ufugaji pia utajifunza dondoo mbalimbali na mbinu bora na za kisasa za ufugaji

Tuesday, October 2, 2018

FURSA KUPITIA TEKNOLOJIA YA KILIMO CHA GREENHOUSE


Karibu sana:
Kwanza tuanze kwa kupata tafsiri ya neno lenyewe, Greenhouse imekua ikipatiwa majina tofauti tofauti, wapo watu wanaiita Nyumba ya Kijani, wengine wanaiita Banda Kitalu n.k Vyovyote utakavyopenda kuiita teknolojia hii, cha muhimu ni kuelewa nini hasa maana yake.

Greenhouse(Banda Kitalu):  ni teknolojia ya kuipatia mimea mazingira mazuri ambayo yataisaidia mimea/mazao kumea vizuri na kua na uzao mkubwa, mimea hii inapandwa kwenye banda, au nyumba maalumu. Teknolojia hii inatumika hasa kuikinga mimea usiathiriwe na mazingira haribifu ya hali ya hewa.

Mazingira haribifu ni kama upepo mkali, baridi kali, mvua kubwa, au mvua za mawe, mionzi mikali ya jua, joto kali , wadudu pamoja na magonjwa. Hayo ndio mazingira ambayo teknolojia hii inaleta suluhisho, kuhakikisha mimea inastawi vizuri bila ya kuathiriwa na moja ya matatizo hayo yaliyotajwa.

Teknolojia hii ilivumbuliwa huko kwenye nchi baridi, zaidi ya karne moja na nusu (miaka 150) iliyopita. Nchi zilizopo ukanda wa baridi, mazao ya kitropiki (mazao yanayo pendelea joto) ilikua haiwezekani kabisa kulimwa maeneo hayo ya ukanda wa baridi. Ndipo hapo wazo la kuvumbua Greenhouse lilipoibuka.

Nchi hizi walianza kutumia teknolojia hii maana nyumba hii ya kijani ilikua ina uwezo wa kutunza joto, na hivyo wakaanza kulima mazao ya ukanda wa joto kama mbogamboga (nyanya, hoho) na matunda. Pamoja na teknolojia hii kuanza kitambo kidogo katika nchi zilizoendelea, lakini kwa upande wa nchi zinazoendelea bado teknolojia hii ni mpya kwa watu wengi.  Teknolojia hii pia inatumika katika nchi za joto, japo kuna utofauti  kati yake na  zile za nchi za ukanda wa baridi.

Faida za Greenhouse

  • Mavuno yanakua mara 10 hadi 12 zaidi ya kilimo cha eneo la wazi, ikitegemea aina ya mazao yanayolimwa humo, aina greenhouse pamoja na vifaa vya kudhibiti mazingira ya ndani ya greenhouse.
  • Uhakika wa kuvuna mazao unaongezeka. Maana Greenhouse inaweza kuzuia visababishi vya  uharibifu wa mazao.
  • Uzalishaji wa mazao katika kipindi chote cha  mwaka, maana huhitaji kusubiri mpaka msimu wa zao ufike ndio ulime.
  • Uwezo wa kupata soko zuri la mazao. Greenhouse itakuwezesha kuzalisha kipindi ambacho sio cha msimu (off- season) kwa vile kipindi hiki watu wengi hawazalishi kutokana na mazingira kutoruhusu,  ukiwa na greenhouse una uwezo wa kuzalisha kipindi hicho na ukapata bei nzuri
  • Ufanisi katika utumaji wa dawa, viwatilifu katika kudhibiti.
  • Matumizi ya maji ni madogo sana na udhibiti  wake  ni rahisi. Miundombinu ya umwagiliaji inayotumika hapa ni umwagiliaji wa matone (drip irrigation) ambapo maji yanakwenda pale penye mmea pekee.
  • Uwezo wa kutunza mimea inayozalishwa maabara kutokana na teknolojia ya tishu (tissue culture technology) mimea inapotoka maabara kabla haijapelekwa shambani inatunzwa kwanza kwenye greenhouse maalumu kwa ajili  ya kuzoea mazingira ya nje kwanza.
  • Uwezo wa kupanda mimea bila kutumia udongo (soilless culture).  Kutokana na changamoto ya magonjwa na vijidudu vya kwenye udongo kama Nematodes, ndipo uvumbuzi  wa teknolojia ya kupanda mimea kwa kutokutumia udongo ulipotokea

Baadhi ya Nchi zinazofanya vizuri kilimo cha  Greenhouse.
Kuna nchi zaidi ya 50 katika dunia ambapo kilimo kinalimwa kwenye greenhouse. Tutaangalia baadhi ya nchi ambazo zimekua zikifanya vizuri kupitia teknolojia hii. Tuanze na Marekani, Marekani ina eneo takribani 4000 hekta ambazo zina greenhouse kwa ajili ya kilimo cha maua,

Marekani kupitia kilimo hicho wanapata pato la zaidi ya Dola bilioni 2.8 (zaidi ya trilioni 5 hela za Tz) kwa mwaka. Nchini Hispania inakadiriwa zaidi 25,000hekta na Italia ni hekta 18,500, zimefungwa  greenhouse kwa kilimo cha pilipili hoho, strawberry, matango, maharagwe machanga,  pamoja na nyanya.

Canada greenhouse ni kwa kilimo cha maua na mboga mboga wakati ambapo hazilimwi kwingine. Mazao maarufu  yanayolimwa kwenye Greenhouse za Canada kama nyanya, matango na hoho.
Uholanzi ni zaidi ya hecta 89,600 zipo nchini ya greenhouse.

Uholanzi sekta ya greenhouse ndio iliyo bora zaidi duniani. Uholanzi ndio nchi inayoongoza kwa teknolojia hii na wamepiga hatua mbali sana. Yapo makampuni makubwa ya Kiholanzi yanayotumia teknolojia hii baadhi yao yapo hapa Tanzania katika kilimo cha maua, matunda, mbogamboga, pamoja na mbegu. Mfano : Kili Hortex, Multi flower, Mount Meru Flower, Enza Zaden, RJK ZWAAN (Q-SEM na AFRISEM)

Israel: 15000 hekta. Israel ndiyo nchi inayoongoza kwa kuuza maua (cut flowers) nje ya nchi. Japokuwa nchi ya Israel eneo lake kubwa ni jangwa. Pia Nchi ya Israel imekua moja ya nchi zilizopo mstari wa mbele katika teknolojia ya umwagiliaji na Greenhouse.

Balton Tanzania yenye makao yake makuu mjini Arusha, ni moja ya kampuni toka Israel zinazofanya vizuri katika sekta hii.

Uturuki: hekta 10,000 zinalimwa maua na mbogamboga kwa kutumia teknolojia hii ya Green house. Saudi Arabia: 90% ya mazao ya yanya na tango yanalimwa kwenye green house.

Misri 10,000 hekta nyanya, matango na pilipili hoho. Teknolojia ya Greenhouse nchini China inakua kwa kasi sana kuliko nchi yeyote   Japokuwa teknolojia hii haijaanza muda mrefu kivile huko China lakini mpaka sasa zaidi ya hekta 48,000 tayari zimefungwa Greenhouse.  Nchi nyingine zinzofanya vizuri barani Asia ni kama  Japan (40,000hekta) na Korea kusini (21,000 hekta).

Aina za Greenhouse.
Greenhouse zinagawanyika makundi mbalimbali kutegemeana na vigezo vifuatavyo:

Aina za Greenhouse kwa  kigezo cha sura/umbile (shape)
Zipo aina aina 8 za greenhouse, hapa nitataja chache tu kwa majina yake ya kitaalamu

  • Quonset Greenhouse
  • Saw tooth type
  • Even span type greenhouse
  • Uneven span type greenhouse

Aina za Greenhouse kwa kigezo cha Matumizi

  • Green house zinazoongeza joto (Hizi ni kwa maeneo ya baridi)
  • Greenhouse zinazopunguza joto (hizi ni kwa maeneo ya joto)

Aina za greenhouse kwa kigezo cha matengenezo yake (construction)

  • Greenhouse za miti (Wooden framed structure)
  • Pipe framed structure (Greenhouse zinazotumia mabomba)
  • Truss/Aluminium framed structure ( Geenhouse zinazojengwa kwa vyuma)

Aina za Greenhouse kwa kigezo  cha aina ya zana za ufunikaji (covering types)
  • Greenhouse zinazofunikwa kwa zana za Vioo (Glass Greenhouse or Screenhouse) )- hizi zinatumika sana maeneo ya baridi kali, ili kutunza joto kwa muda mrefu ndani   greenhouse
  • Greenhouse zinazofunikwa kwa mifuko ya plaski (plastic film)

Aina ya Greenhouse kwa kigezo cha uwekezaji unaofanywa:

  • Greenhouse za gharama kubwa (High cost greenhouse) ( Zaidi ya milioni 50)
  • Greenhouse za gharama za kati (medium cost greenhouse) (milioni 20 hadi 50)
  • Greenhouse za gharama ndogo (Low cost greenhouse) (chini ya milioni 20)
  • Greenhouse za gharama ndogo ndio watu wengi wanazitumia sana katika nchi zinazoendelea.

No comments:

Post a Comment