USHAURI; Jinsi Ya Kutengeneza Biashara Isiyokutegemea Wewe Moja Kwa Moja Na Kupata Uhuru Wa Kibiashara. - KILIMO NA UFUGAJI

Latest

Karibu uweze kujifunza na kujipatia elimu kuhusiana na kilimo na ufugaji ambapo utajifunza mbinu bora za kilimo na ufugaji pia utajifunza dondoo mbalimbali na mbinu bora na za kisasa za ufugaji

Tuesday, October 2, 2018

USHAURI; Jinsi Ya Kutengeneza Biashara Isiyokutegemea Wewe Moja Kwa Moja Na Kupata Uhuru Wa Kibiashara.


1. Usianze biashara bila ya kuwa na ndoto kubwa.
Sababu moja kubwa inayowafanya wafanyabiashara kubaki kwenye utumwa wa biashara kwa miaka mingi ni ndoto zao za kibiashara. Wengi wamekuwa wakianza biashara kama sehemu ya kutengeneza kipato cha ziada. Kwa hiyo wanapotengeneza kipato hicho cha ziada hakuna kingine kikubwa kinachowasukuma, hivyo wanaishia hapo.

Unahitaji kuwa na ndoto kubwa za kibiashara, unahitaji kuiona biashara yako ikikua na kuwasaidia watu wengi zaidi kuwa n amaisha bora. Ndoto hii kubwa ndiyo itakusukuma na kutengeneza biashara inayojitegemea.

Unaruhusiwa kuanza biashara kidogo, lakini usianze biashara bila ya kuwa na ndoto kubwa. Uzuri wa ndoto ni bure, hakuna anayekutaka ulipie ndoto kubwa ulizonazo, hivyo jiwekee ndoto kubwa za biashara yako, jinsi itakavyokuwa kubwa na kugusa maisha ya wengine.

2. Tengeneza mifumo ya biashara mapema kabla hata hujaihitaji. 
Tatizo jingine kubwa kwenye biashara ndogo na za kati ni kukosekana kwa mfumo wa biashara. Wengi wamekuwa wakifikiria kwamba biashara ni kuuza na kununua, au kutengeneza na kuuza. Hivyo wanapeleka nguvu zao maeneo hayo, wanajikuta wametingwa kila siku, lakini hawaoni hatua kubwa wanazopiga.

Unapoiendesha biashara nzima kama kitu kimoja, biashara haiwezi kujitegemea, kwani ni wewe pekee unayeweza kuielewa biashara hiyo vizuri. Ukiajiri mtu mwingine hawezi kuielewa vizuri kama wewe na hivyo kukutana na changamoto.

Tengeneza mifumo inayoeleweka ya biashara yako, ambapo majukumu kwenye mifumo hiyo yanaweza kupewa watu wengine. Kwa kuanzia na kwa biashara ndogo na za kati, angalau weka mifumo mitatu. Uzalishaji, usimamizi na masoko na mauzo. Kwenye uzalishaji hapa ndipo bidhaa au huduma inaposimamiwa katika manunuzi au matengenezo. Masoko na mauzo hapa ndipo biashara inamfikia mteja wako, usimamizi hapa ndipo shughuli zote za biashara zinaposimamiwa.

3. Ajiri watu bora na waamini. 
Kitu kingine kinachowafanya wafanyabiashara wadogo na wakati kuwa watumwa wa biashara zao, ni pale wanapofikiri kwamba hakuna mtu anayeweza kuendesha biashara zao vizuri kama wao wenyewe. Hali hii inawazuia kuweza kuajiri watu ambao wangeweza kuwasaidia kuendesha biashara zao, hivyo kukazana kufanya kila kitu wao wenyewe.

Unahitaji kuajiri wafanyakazi bora, kisha kuwaamini kwamba watatekeleza majukumu yao na kuwakabidhi majukumu hayo. Ukishaajiri haimaanishi ndiyo umemaliza, badala yake unaendelea kufuatilia kwa karibu ili kujua maendeleo ya biashara yako yanakwendaje, hasa kwa maeneo hayo ambapo umeajiri.

Muhimu hapa ni kupata wafanyakazi bora, na siyo bora wafanyakazi. Kwa sababu wafanyabiashara wengi, wamekuwa wakiajiri watu ambao wanataka mshahara kidogo, mara nyingi watu hawa wanakuwa siyo bora kwa ukuaji wa biashara yako.

4. Usiajiri mtu, ajiri nafasi. 
Hapo juu tumeshaona kwamba unahitaji kuajiri watu watakaoweza kukusaidia kuendesha biashara yako. Hapa tutaangalia jambo moja muhimu sana katika kuajiri, kwa sababu hapa ndipo makosa makubwa sana yamekuwa yanafanywa na kuwaathiri wafanyabiashara wengi.

Wafanyabiashara wadogo na wa kati, wamekuwa wanaajiri mtu. Yaani wanamwajiri mtu, halafu akifika kwenye biashara ndiyo wanamfikiria anaweza kufanya shughuli zipi. Hii ni hatari kubwa kwa sababu siku akiondoka, ni vigumu kumpata mwingine kama yeye na hivyo biashara yako inatetereka.

Katika kuajiri, usimwajiri mtu halafu akifika ndiyo uangalie anaweza kufanya nini, badala yake ajiri nafasi za kazi. Yaani mwajiri mtu ukiwa tayari una majukumu ambayo anapaswa kuyatimiza, kulingana na mfumo wa biashara yako. unaweza kuajiri mtu kwa ajili ya uzalishaji, au masoko na mauzo na kadhalika. Muhimu ni kuhakikisha mfanyakazi anayajua majukumu yake kwenye biashara yako, na hata watakapotaka kuondoka, unaweza kupata wengine wa kuziba pengo lao.

5. Gawa majukumu yako kwa wengine. 
Changamoto kubwa sana kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati ni kung’ang’ania kufanya kila kitu wao wenyewe. Wakati mwingine wanafanya hivi wakiamini wanaweka ubora zaidi, wakati mwingine wanafanya hivi kuepuka gharama za kuwalipa wengine.

Lakini kuna vitu viwili ambavyo una uhaba navyo na ni muhimu sana kwako, muda na nguvu. Haijalishi una hamasa kubwa kiasi gani ya kufanya shughuli zako, kuna masaa 24 pekee kwenye siku yako, huwezi kuongeza hata dakika moja. Pia kadiri unavyofanya mambo mengi, mwili wako unachoka na nguvu zinatumia.

Kuondokana na hali hii, orodhesha majukumu yako yote kisha angalia ni majukumu yapi ambayo yanakuhitaji wewe kweli. Yale mengine ambayo kuna watu wanaweza kuyafanya vizuri, watafute watu hao na wayafanye. Siyo lazima uwe umeajiri watu hao, unaweza kuwapa wakufanyie kama vibarua au kwa mikataba maalumu.

Lengo kuu la kuanzisha biashara ni kupata uhuru wa kipato na muda, sasa kama biashara inakuwa inakutegemea wewe moja kwa moja, bado hujaweza kutengeneza uhuru wako kwenye muda na kipato. Fanyia kazi haya tuliyojifunza hapa na utaanza kuona mabadiliko kwenye biashara yako.

No comments:

Post a Comment