Kilimo Bora Cha Bilinganya Nyeupe - KILIMO NA UFUGAJI

Latest

Karibu uweze kujifunza na kujipatia elimu kuhusiana na kilimo na ufugaji ambapo utajifunza mbinu bora za kilimo na ufugaji pia utajifunza dondoo mbalimbali na mbinu bora na za kisasa za ufugaji

Sunday, May 28, 2017

Kilimo Bora Cha Bilinganya Nyeupe

                        

Zao lenye pato kubwa
Bilinganya nyeupe (Long White Eggplant) ni moja ya zao la mbogamboga ambalo lina viini lishe vingi na muhimu kama vile madini aina ya chokaa na chuma, Vitamini A, B na C, wanga, protini na maji
Kisayansi zao hili hujulikana kama Solanum Melongenai na kilimo chake huweza kufanyika katika majira yote ya mwaka.
Hali ya Hewa
Zao hili huhitaji hali ya joto la wastani, udongo wenye kina kirefu na rutuba ya kutosha na usiotuamisha maji. Kwa kawaida bilinganya hulimwa zaidi ya msimu mmoja, lakini katika nchi za kitropiki (joto) zao hili hulimwa kwa msimu mmoja.
Udongo
Zao la hili huota katika udongo wa kichanga na tifutifu, wenye rutuba ya kutosha. Unashauriwa kuweka mboji katika shamba lako ili kuurutubisha udongo vizuri.
Utayarishaji wa kitalu na usiaji
Ni muhimu kusia mbegu katika trei ili kukwepa kupotea kwa miche pamoja na kupata miche bora. Miche huchukua siku saba hadi kumi kuchipuaa, na wiki tatu hadi nne kwenye kitalu, kisha kupelekwa shambani. Ikiwa mkulima atasia mbegu ardhini, ni vyema kuandaa eneo lenye mbolea ya kutosha. Waweza kuweka mbolea ya mboji katika eneo hilo au katika matuta yako uliyoyaandaa kwa ajili ya kusia mbegu.
Upandaji wa miche
Unapopeleka miche yako shambani, hakikisha unaotesha kwa kufuata maelezo muhimu ya utaalamu ili kuweza kupata mavuno mengi na yenye ubora. Matuta ya kunyanyua yasiyotuwamisha maji hushauriwa kutumika katika kilimo cha zao hili kwani huzuia kuoza kwa mimea maji yanapotuama. Nafasi kati ya mche na mche iwe sentimeta 60 huku nafasi kati ya mstari na mstari iwe ni hatua moja. Hakikisha shamba limemwagiliwa na weka mbolea ya mboji katika kila shimo wakati wa kuotesha.
Umwagiliaji
Zao hili likipata maji ya kutosha husitawi vizuri hivyo ni muhimu kumwagilia mara mbili hadi tatu kwa wingi kulingana na msimu husika hasa wakati wa kiangazi. Usimwagilie kipindi cha mvua kwani utasababisha bilinganya kuoza kutokana na wingi wa maji.
Palizi
Hakikisha unafanya palizi mara kwa mara na kuacha shamba likiwa safi wakati wote ili kuondoa ushindani wa magugu na mimea kwenye chakula, maji na mwanga. Pia kuzingatia usafi kutasaidia kupunguza kuzaliana kwa wadudu waharibifu pamoja na magonjwa.
Magonjwa na wadudu
Zao hili hushambuliwa na wadudu pamoja na magonjwa ya aina mbalimbali hasa linapolimwa wakati wa kiangazi.
Utitiri: 
Wadudu hawa kwa kiasi kikubwa wamekuwa visumbufu vya zao hili na si rahisi kukuta bilinganya haijashambuliwa na wadudu hawa, hasa wakati wa joto au kiangazi.
Kimamba: Hawa wadudu pia hushambulia bilinganya mara kwa mara wakati wa kiangazi.
Inzi weupe (white flies): 
Wadudu hawa kwasasa ni visumbufu vya mazao mengi ya bustani ama ya mbogamboga, na bilinganya ni moja ya mazao yanayoshambuliwa na wadudu hawa kwa kiasi kikubwa. Bilinganya inapoanza kuzaa matunda, wadudu hawa huvamia na hujikita katika majani, hufyonza maji na hatimaye bilinganya hukauka. Wadudu hawa hueneza ugonjwa unaofahamika kwa jina la Rasta. Huweza pia kusababisha majani kubadilika rangi na kuwa meusi
Barafu: 
Huu ndio ugonjwa mkubwa unaosumbua zao la bilinganya, na mara nyingi ugonjwa huu hutokea kipindi cha mvua. Husababisha tunda ya bilinganya kupata ukungu, kuoza na kudondoka kwenye mti. Na inaposhika tunda moja, ni rahisi kuambukiza lingine kwa haraka na matunda ya mti wote hushambuliwa. Pia wadudu kama leaf miner, bollworm, beetle pamoja na magonjwa kama root rot, leaves sports , kutu, kuoza kwa tunda, bakajani hushambulia zao hili pia.
Namna ya kudhibiti
Wadudu huweza kudhibitiwa kwa kutumia mwarobaini, tumbaku, majivu na mafuta ya taa, majani ya mustafeli pamoja na mfoori kulingana na vipimo na namna ya utengenezaji kwa maelezo sahihi kutoka kwa mtaalamu wa kilimo. Ikiwa mkulima atatumia viuatilifu, ni muhimu kutumia kulingana na ushauri wa wataalamu. Pia kuepuka kulima zao hili katika msimu ambao wadudu hao wanakuwepo kwa kasi hasa kipindi cha kiangazi.
Mavuno
Kwa wastani, bilinganya nyeupe hutoa kilogramu 10,000 hadi 15,000 kwa ekari moja. Aina hii ya bilinganya haina tofauti sana na aina nyingine kwani huchukua siku 80 hadi 95 kukomaa na kuanza kuvunwa. Kiwango cha mavuno huongezeka mchumo baada ya mchumo, kadri siku zinavyoendelea na pia kulingana na matunzo. Bilinganya hutoa mavuno mengi na bora kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo, baada ya hapo mavuno huwa hafifu.
Matumizi
Mboga hii hutumika kwa ajili ya kutengeneneza saladi japo wengine pia hutumia kama mboga au kama kiungo cha chakula.

No comments:

Post a Comment