Banda la kulelea vifaranga - KILIMO NA UFUGAJI

Latest

Karibu uweze kujifunza na kujipatia elimu kuhusiana na kilimo na ufugaji ambapo utajifunza mbinu bora za kilimo na ufugaji pia utajifunza dondoo mbalimbali na mbinu bora na za kisasa za ufugaji

Sunday, September 24, 2017

Banda la kulelea vifaranga

Ukipenda kujenga nyumba ya vifaranga itafaa ufikirie yafuatayo:-

  1. Nyumba ya vifaranga iwe karibu na nyumba yako mwenyewe ili uweze kuwakagua vifaranga wako mara kwa mara.
  2. Ijengwe hatua 20 au zaidi mbali na nyumba ya kuku wakubwa, hii ni kinga mojawapo ya kupunguza hatari ya maambukizi ya magonjwa.
  3. Nyumba ya vifaranga isiruhusu ubaridi au unyevu au wanyama waharibifu kuingia. Lakini nyumba iingize hewa na mwanga wa kutosha kila wakati.
  4. Nyumba iwe na eneo la kutosha ili vifaranga wapate nafasi ya kutembea kutafuta chakula na maji bila kubanana.
  5. Ijengwe kwenye sehemu isiyoelekea upepo unaotoka kwenye nyumba ya kuku wakubwa. Tahadhari hii husaidia vifaranga kuepukana na magonjwa yanayoenezwa na upepo.



Eneo: Vifaranga hawahitaji eneo kubwa katika muda wa majuma 4 ya kwanza. Nafasi inayohitajiwa kwa kukadiria ni meta za eneo 1 kwa kila vifaranga 16. Kwa mfano nyumba yenye Meta 10 za mraba inatosha kulea vifaranga 160 hadi umri wa majuma 4. Vipimo vya nyumba yenye eneo kama hili inaweza kuwa na hatua 5 kwa hatua 4 au hatua 3 kwa 3.25. Utajenga kutegemea na eneo ulilonalo. Baada ya majuma 4 ya umri ongeza nafasi na uwape vifaranga eneo la kuwatosha.

Sakafu: Sakafu nzuri katika nyumba ya vifaranga ikiwezekana inafaa ijengwe na simenti iliochanganywa na zege. Ili kupunguza gharama, unaweza kutumia vifaa vya ujenzi vinavyopatikana kirahisi katika eneo lako vitumikavyo kusiriba sakafu kama udongo wa kichuguu au unaweza kulainisha kinyesi cha ng’ombe kwa maji na kusiriba eneo lote la sakafu.

Ukuta: Ingefaa kuta za nyumba za kulea vifaranga za matofali, udongo, mabati au debe. Kuta za matofari na udongo zipigwe lipu ili kurahisisha usafishaji wa nyumba au umwagiaji wa dawa. Urefu wa kuta uwe tangu meta 1.8 – 2.4 (futi 6-8). Sehemu ya kutoka chini ya meta 0.9 – 1.2 (futi 3 – 4) izibwe na ukuta wa tofali au udongo na sehemu ya juu iliyobakia yenye meta 0.9 – 1.2 (futi) 3-4) ijengwe kwa wavu wa chuma au fito.

Mbao: Nguzo za miti au mbao zilowekwe dawa ya mbao kama vile “Dudu killer” au oili chafu ili kuzuia kuoza. Ukitumia miti ni vizuri uondoe magome ambayo yanaweza kuweka vimelea na wadudu.

Madirisha: Unaweza kutumia maboksi, mikeka ya magunia, mapazia ya magunia ni rahisi na yanaweza kuwekwa kwa kupigiliwa misumari kwenye dari na upande wa chini pazia ipigiliwe misumari kwenye ubao ili ininginie.Unaweza kukunja mapazia/magunia ili uingize hewa na mwanga wa kutosha katika nyumba ya vifaranga.

Paa: Mjengo wa paa uwe unaoweza kuwapatia vifaranga hewa ya kutosha hivyo paa liwe na tundu la kutoa nje hewa yenye joto. Kwa kadri utakavyoweza, unaweza kutumia madebe, mabati, makuti au nyasi n.k. kuezeka nyumba ya vifaranga. Sehemu ya paa ikianza kuvuja iezekwe bila kuchelewa.

No comments:

Post a Comment